
Kitendo hicho kilifanyika Jumapili licha ya polisi wa eneo hilo kupiga marufuku tukio hilo la uchochezi na kumwonya Paludan kufuatia kuuawa kwa Salwan Momika, raia wa Iraq aliyejulikana kwa kuandaa maandamano yanayofanana nchini Sweden.
Paludan, kiongozi wa chama cha mrengo mkali wa kulia Stram Kurs, alichapisha video ya tukio hilo kwenye mtandao wa X, akidai kuwa ni heshima kwa Momika na pia ni kushinikiza polisi wa Denmark waliomzuia yeye na chama chake kufanya maandamano.
Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya mamlaka za Denmark, zikiwemo idara za kijasusi (PET), kuwasiliana na Paludan kufuatia kuuawa kwa Momika katika nyumba moja mjini Södertälje, Sweden, Alhamisi usiku.
Momika alipata umaarufu kwa kuchoma nakala za Qur'ani Tukufu hadharani, vitendo vilivyopingwa kimataifa na kusababisha hasira kubwa miongoni mwa Waislamu.
Uchochezi mpya wa Paludan dhidi ya Waislamu unakuja wakati ambapo bunge la Denmark lilipitisha sheria inayopiga marufuku uchomaji wa Qur'ani hadharani.
Sheria hiyo, inayozuia “matumizi yasiyofaa ya maandiko yenye umuhimu wa kidini kwa jamii inayotambulika kisheria”, ilipitishwa Desemba 2024 kwa kura 94 dhidi ya 77 katika bunge la Denmark lenye viti 179 (Folketing).
Katika utekelezaji wa sheria hiyo, itakuwa haramu kuchoma, kurarua, au kunajisi maandiko matakatifu hadharani au kupitia video zinazosambazwa kwa umma. Wanaokiuka sheria hiyo watakabiliwa na faini au kifungo cha hadi miaka miwili jela.
Denmark na Sweden zilishuhudia msururu wa maandamano mwaka 2023, ambapo wanaharakati wa chuki dhidi ya Uislamu walichoma au kuharibu nakala za Qur'ani, hali iliyosababisha mvutano mkubwa na mataifa ya Kiislamu pamoja na shinikizo la kupigwa marufuku kwa vitendo hivyo.